TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

TANZANIA YACHAGULIWA KUWA RAIS WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARRIBEAN NA PACIFIC

Dodoma, 6 Agosti 2020

Serikali ya Tanzania imechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacific (Organisation of African, Carribean and Pacific States-OACPS)  kwa kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 1 Agosti 2020 hadi tarehe 31 Januari 2021.

Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikabidhiwa rasmi nafasi hiyo iliyopokelewa kwa niaba yake na Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro,  Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 28 Julai 2020.

Tanzania inakuwa Rais wa Baraza hilo kutokana na Balozi  wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za OACPS waliopo Brussels. Kwa mujibu wa Jumuiya ya OACPS,  nchi inayotoa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Jumuiya hiyo, Waziri wake anayesimamia masuala ya OACPS ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje moja kwa moja anakuwa Rais wa Baraza la Mawaziri. Uamuzi wa kuichagua Tanzania ulifanywa na Mabalozi kutoka nchi 15 za Ukanda wa Mashariki mwa Afrika kwenye kikao kilichofanyika tarehe 2 Julai 2020 na kuthibitishwa kwa kauli moja na mabalozi wote wa nchi 79 wa OACPS kupitia kikao chao kilichofanyika Brussels tarehe 14 Julai 2020.

Tanzania ambayo inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gambia, imejipanga kutekeleza masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Nchi za OACPS ikiwa ni pamoja na kusimamia ukamilishwaji wa majadiliano kuhusu Mkataba mpya wa ushirikiano wa Nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya (EU) unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi Januari 2021 baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou (Cotonou Partnership Agreement) kufikia ukomo mwezi Desemba 2020, pamoja na kuhakikisha  maslahi ya nchi za OACPS yanaingizwa kwenye mkataba huo mpya. Aidha, Tanzania imejipanga kusimamia utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya Jumuiya ya OACPS katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID-19 na madhara yake kiuchumi kwa nchi wanachama.

 Kadhalika, maeneo mengine ya kipaumbele yatakayosimamiwa na Tanzania katika kipindi cha Urais wa Baraza hilo ni kusimamia  mikakati ya kuongeza mtangamano na ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya; kusimamia mabadiliko ya kiutendaji na mifumo ili kuendana na wakati pamoja na kudumisha mshikamano na umoja miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya.

 Vilevile miongoni mwa manufaa ya Tanzania kuwa Rais wa Baraza hilo  ni pamoja na kuongeza ushawishi wa nchi yetu katika kupanga na kutekeleza mikakati, miradi na programu mbalimbali za Jumuiya ya OACPS ambazo ni pamoja na zile zinazotekelezwa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya na wabia wengine wa maendeleo kama vile kilimo, uwekezaji, biashara na ujasiriamali, mazingira, miundombinu, vijana na utamaduni.

 Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS tangu ilipojiunga mwaka 1975. Miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo ni kutokana na kuongozeka kwa ushawishi wake kwenye Jumuiya ya OACPS, Sera na hatua thabiti zinazochukuliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pamoja na utendaji madhubuti wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kusimamia Sera ya Mambo ya Nje  ikiwemo ushiriki mahiri wa Tanzania katika masuala yanayogusa maslahi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya OACPS.

  

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali.